NA DODI SIFI ULE msemo usemao ‘Kupiga ndege wawili kwa jiwe moja’ unaendelea kuishi katika jamii zetu ambapo ni dhahiri ...
NA DODI SIFI
ULE
msemo usemao ‘Kupiga ndege wawili kwa jiwe moja’ unaendelea kuishi katika jamii
zetu ambapo ni dhahiri unasadifu maisha ya Peter Njovu mwenye miaka 86 kutokana
na jinsi anavyoendesha maisha yake.
Njovu
ambaye alizaliwa mwaka 1930 kila siku asubuhi hukaa kibarazani kwake kuota jua kwa
ajili ya kupata Vitamini D huku akichonga mihuri kazi anayoifanya kwa ustadi
mkubwa ukilinganisha na umri wake na kujipatia fedha za kuendesha maisha yake.
Peter
Njovu linaweza likawa si jina geni kwa walimu na watumishi wa serikali wa miaka
ya 1970 na 1980. Alikuwa mtumishi wa serikali katika sekta ya elimu (mwalimu)
tangu mwaka 1954 kabla ya kupanda ngazi na kuwa mratibu wa vyuo vya ufundi
Tanzania katika kipindi cha miaka mitatu kutoka 1973 hadi 1976.
Mzee Njovu akiendelea na kazi ya kuchonga mihuri huko Kibamba jijini Dar es Salaam |
Njovu
pia ni msanii wa uchoraji na aliwahi kuchora picha maarufu ya Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere ambayo huonekana katika ofisi za Umma na hoteli mbalimbali.
Tunaweza kusema mzee huyu amaeacha alama nzuri katika Taifa la Tanzania.
“Kazi hii ya uchongaji na uchoraji nilianza
nikiwa mdogo kabla sijaenda shule. Baada ya kustaafu kazi ya ualimu, nilianza
tena uchongaji wa mihuri kutokana na ukiwa nilionao, mke wangu ameshafariki,
watoto wangu wote wana miji yao, naishi peke yangu.
Kazi
hii naichukulia kama sehemu ya kuondoa ukiwa lakini pia inanipatia pesa nzuri
tu. anasema kwa masikitiko.
Siwezi
kukaa bila kufanya kazi, kazi zote ndani ya nyumba yangu nazifanya mimi, usafi,
kupika, hata kulima. Nikiwa na muda wa mapumziko nachukua kitabu au gazeti
nasoma, hii ni kutokana na tabia niliyojijengea awali nikiwa mwanafunzi hata
nilipokuwa mwalimu”.
“Mimi nilichelewa sana kuanza shule kutokana
na uchache wa shule pamoja na wazazi wetu kutokuwa na hamasa ya kupenda
kuwapeleka watoto shule. Walipenda watoto wafanye kazi za mashambani na kutunza
mifugo.
Anasema
kilichomfanya aandikishwe shuleni ni kutokana na kipaji alichonacho hususan
katika sanaa ya uchongaji na uchoraji. “Nikiwa kijana wa miaka 10 nilianza
kuchonga vinyago na kuchora fani ambayo nimezaliwa nayo,Kutokana na umahiri
wangu katika sanaa ya uchongaji na uchoraji , bidhaa zangu zilipendwa sana na
Wazungu waliokuwa wafanya kazi katika misheni ya Peramiho ambao ndio walikuwa
wateja wetu,”.
Kwa
mujibu wa mzee Njovu wazungu hao walivutiwa na sanaa yake na kuamua kufika nyumbani
kwao kwa lengo la kuwashawishi wazazi wampeleke shule kuendeleza kipaji chake
ambapo walikubali”. Anasema.
Anasema
baada ya wazazi wake kuridhia ombi la wazungu mwaka 1945 alianza darasa la
kwanza katika shule ya msingi Peramiho akiwa na miaka 15.
“Kutokana
na umri mkubwa ilibidi nirushwe darasa la kwanza na la pili ambayo alisoma kwa mwaka
mmoja, pia sikuweza kusoma na kuandika vizuri,lakini nilikuwa nafanya mitihani
na kufaulu vizuri darasani kwasababu nilikuwa na changamoto kubwa ya kushindwa kujieleza
kwa kujibu maswali badala yake nilitumia sanaa yangu ya uchoraji kujibu
maswali, na nilikuwa nikijibu kila mtihani kwa kutumia picha,”.
Anasma
mwaka 1948 kati ya wanafunzi 32 walifanya mtihani wa darasa ya nne waliofaulu
walikuwa wanne tu Njovu akiwa mmojawapo na kumfanya kuchaguliwa kujiunga na
chuo cha ufundi hapo hapo Peramiho mwaka 1951 ambapo alisomea masomo ya
uchongaji, uchoraji, useremala, na ufinyanzi.
1951-1953
alijiunga na chuo cha ualimu Peramiho ngazi ya diploma na alipomaliza tu akaanza kufundisha chuoni
hapo (1954).
“
Mimi nilikuwa mwalimu tofauti sana nilikuwa napenda kubadilisha mazingira ya
kutoa elimu yangu, nilikuwa naomba serikali inihamishie katika shule za awali,
msingi na vyuo vya ufundi, hii ni kutokana na mapungufu yaliyokuwa yanajitokeza
katika sehemu nyingi na kuhitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka. Nilikuwa
nazunguka mikoa ambayo ilikuwa nyuma kielimu, ili kubadilisha hali hiyo”
Baadhi
ya vyuo alivyowahi kufundisha ni Chuo cha Ualimu Katoke, Kasulu, Mpwapwa,
Tabora, Mara na Tanga.
Anasema
mmoja wapo kati ya wanafunzi aliowafundisha ni jaji mkuu mstaafu wa Tanzania
Barnas Samatta.
Pia
Njovu anasema mwaka 1970 alipata ufadhili wa kwenda kusoma Korea Kaskazini
katika sanaa ya ufundi lakini kutokana na hali ya hewa ya nchi hiyo ilibidi arudi
nyumbani Tanzania kwa ajili ya kumalizia masomo katika chuo kikuu cha Dar es
Salaam.
Mwaka
1974 hadi 1976 alifanya kazi ndani ya Wizara
ya elimu kama mratibu wa vyuo vya ufundi Tanzania lakini kutokana na mapenzi yake
katika ufundishaji aliomba serikali imrudishe katika ufundishaji.
“Mwaka
1976 hadi 1980 nilifundisha katika chuo cha ualimu cha Mara. Na mwaka 1980 hadi 1984 nilikuwa
nafundisha vyuo viwili , Kasulu na Kabanga vyote vipo mkoani Kigoma.
SIRI YA UMRI
WAKE
Njovu
anasema siri kubwa ya kuwa na umri wa miaka 86 ni mapenzi ya Mungu kumuweka
mpaka sasa lakini pia ni kutokana na kujitunza kwake hususan katika maswala ya
vyakula ambavyo vinamfanya azidi kuishi akiwa na afya njema na nguvu.
Anasema
yeye hupendelea zaidi vyakula vya asili hasa mboga mboga zaidi mchunga na
matunda.
Kingine
ambacho ni kubwa zaidi katika kuimarisha afya katika umri wake wake huo Njovu
anasema hutembea umbali kiasi cha kilometa 7 hadi 10 kwenda na kurudi, wakati
akisambaza bidhaa alizotengeneza (mihuri) kwa wateja wake.
Njovu
ambaye ni mkazi wa Kibamba hutemebea hadi Kibaha, Bagamoyo na vijiji jirani.
LUGHA
Licha
ya Kiswahili ambacho n dio Lugha mama lakini Njovu anamudu kuzungumza lugha ya
Kikorea, Kichina, Kiingereza pamoja na baadhi ya lugha za asili za makabila ya
ukanda wa kaskazini na Kenya.
MAISHA YA NDOA
Njovu
alifanikiwa kuoa mke ambaye kwasasa ni marehemu mwaka1964 ambaye pia alikuwa
mwalimu na walibahatika kupata watoto 8 wasichana wanne na wavulana wanne hata
hivyo anaishi peke yake kwa sasa kutokana na watoto wake wote kuwa wanajitegemea.
Licha
ya kuwa na umri huo lakini Njau anasema kuwa anajipikia mwenyewe chakula kwani
kwake ni suala dogo na ameshazoea kwa maidai kuwa alichelewa kuoa.
Hata
hivyo Njovu anasema pia alikuwa mwalimu wa muziki kama somo la ziada, fani
ambayo aliimudu vizuri katika kuimba na kupiga ala za muziki zikiwemo kinanda,
tarumbeta, na saxophone.
Njovu anamaliza kwa kutoa rai kwa vijana kufanya
kazi kwa bidii na kuzingatia sana katika maadili ya kijamii pamoja na kujali
afya zao kwa kupenda kufanya mazoezi na kusoma vitabu mbalimbali ili
kujiongezea maarifa
COMMENTS