MKOA wa Morogoro ni mojawapo ya maeneo hapa nchini yanayokua kwa kasi kiuchumi kupitia shughuli za uzalishaji mali, kilimo na biashara...
MKOA wa Morogoro ni mojawapo ya
maeneo hapa nchini yanayokua kwa kasi kiuchumi kupitia shughuli za uzalishaji
mali, kilimo na biashara na hivyo kuwa miongoni mwa maeneo hapa nchini
yanayochangia uchumi wake katika pato la Taifa.
Tathmini inaonyesha kuwa ukuaji wa
uchumi mkoani humo unakwenda sambamba na ongezeko la watu na hivyo kuwapo kwa
hitaji kubwa la mazingira yanayorahisisha utekelezaji wa shughuli za uzalishaji
na uendeshaji wa biashara hasa kundi kubwa la wafanyabiashara ndogondogo,
maarufu kama wamachinga.
Pamoja na mchango mkubwa wa biashara
ndogo ndogo kufikia wastani wa zaidi ya ajira milioni 5 hapa nchini,
wafanyabiashara mkoani Morogoro na maeneo mengine nchini wanakabiliwa na tatizo
la maeneo ya kuendesha biashara zao.
Pamoja na changamoto hiyo, migogoro
kati ya wafanyabiashara ndogondogo na mamlaka imetajwa kuwa kikwazo cha
maendeleo ya biashara ndogondogo mkoani humo.
Chanzo cha mgogoro uliodumu kwa
zaidi ya miaka miwili sasa kimetajwa kuwa ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini
Morogoro kuwataka wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao kwenye eneo la Sabasaba, Halmshauri ya Manispaa ya
Morogoro kukilipa chama hicho kodi ya pango huku wafanyabiashara hao wakigoma
kwa maelezo kuwa eneo hilo sio mali ya CCM.
Wafanyabiashara
hao zaidi ya 50 wanakilaumu CCM wilayani humo kuwa chanzo cha umasikini kwa
kuzusha migogoro ambayo imesababisha wafanyabiashara wengi kukosa haki ya
kufanya shughuli zao kwa uhuru, huku wakimtupia lawama Katibu wa CCM wilayani
humo Ally Issa.
Wanamlalamika
kutumia cheo chake kuwanyang’anya mabanda yao
ya biashara jambo ambalo limewaathiri kwa kiasi kikubwa katika shughuli
zao.
Wanadai
kuwa walipatiwa eneo hilo na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kutokana na
maeneo hayo kuwa wazi ambapo kwa makubaliano maalumu waliridhiana na uongozi wa
Manispaa ya hiyo kujenga mabanda na kuendesha biashara zao kwenye maeneo rasmi
baada ya wafanyabiashara wengi kulazimika kuendesha biashara zao kwenye maeneo
yasiyoruhusiwa kwa kukosa maeneo ya kufanya biashara zao.
Wanasema
katika hali ya kushangaza uongozi wa CCM wilaya ya Morogoro mjini walifika
kwenye eneo hilo na kuanza kuwatoza kodi
huku wakitishia kuwafukuza wafanyabiashara watakaokaidi ikiwa ni pamoja
na kunyang’anywa mabanda wanayoyatumia kuendesha biashara zao.
Akizungumzia
kadhia hiyo kiongozi wa wafanyabiashara hao Robert Mluge anasema waliazimia
wote kugoma kutozwa kodi kwa maelezo kuwa maeneo hayo ya wazi ni mali ya
serikali na yanasimamiwa na Manispaa ya Morogoro na siyo mali ya CCM kama
uongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya unavyodai.
“Katibu
wa wilaya wa CCM alivyoona tumegoma kulipa kodi, walikuja na kuamuru kufunga
mabanda yote, baada ya siku chache Katibu Ally alitoa amri yavunjwe ili CCM
itafute watu wengine na kuwapa maeneo hayo… kwa kweli tuliumia sana,” anasema
Mluge.
Anasema
kuwa watekelezaji wa agizo hilo waliuza mali za wafanyabiashara zilizokuwamo
ndani ya mabanda huku CCM ikiyakodisha kwa wafanyabiashara wengine kwa nguvu.
“Sisi
tuliingia makubaliano na Halmashauri ya Manispaa tukapewa maeneo tujenge
mabanda yetu lakini tulitakiwa tutumie gharama zetu kwanza kujenga uzio kabla
kufanya jambo lolote ili kuimarisha usalama wa eneo hilo lakini cha kushangaza
CCM waliingilia jambo hili pasipo sababu za msingi,” alisema Mluge.
Mluge
anasema katika kutafuta haki walifungua kesi katika mahakama ya ardhi dhidi ya
CCM wilayani hapo ambapo wafanyabiashara walishinda kesi hiyo. Hata hivyo
pamoja na ushindi huo CCM walipuuza hukumu ya mahakama ya kuwataka kurudisha
vibanda hivyo kwa wafanyabiashara wenye haki. Hadi sasa mabanda hayo
yanaendelea kushikiliwa na wafanyabiashara waliowekwa na CCM.
Anasema
baada ya kuona kila njia wanayotumia kutatua tatizo hilo inakwama, waliamua
kumtumia barua Katibu Mkuu wa CCM taifa, Abdulrahman Kinana ili aimuru CCM
wilayani humo kuheshimu sheria na mahakama lakini hadi sasa hakuna ufumbuzi
wowote.
“Maisha
yetu na familia yanalikuwa yakitegemea vibanda tulivyonyang’anywa, hivi sasa
tunakosa ada ya shule kwa watoto wetu, mahitaji ya msingi nyumbani na mengine
ya kijamii,” analalama Mluge.
Mfanyabiashara
mwingine, Lazarus Mizambwa anasema imekuwa ni jambo la kushangaza kwa chama
ambacho kinasema sera zake ni za kuondoa umasikini kikiwa mstari wa mbele kuwakandamiza
wafanyabiashara wadogo ambao wamekuwa muhimu kwenye maendeleo ya jamii na pato
la taifa kwa ujumla.
“Inashangaza
sana, hiki ndicho chama ambacho kinaiaminisha jamii kwamba kina sera nzuri za
kupunguza au kuondoa umasikini kwa kuandaa mkakati wa kukuza uchumi na kuondoa
umasikini (Mkukuta), lakini kinaibadili mikakati hiyo ya kuongeza umasikini kwa
wananchi kama hivi,” anasema Mizambwa.
Naye
Flexon Lauo anasema kitendo hicho cha kibabe cha kunyang’anywa maeneo yao ya
biashara kinawafanya wana jamii kupoteza imani na chama hicho kikongwe hapa nchini.
“Kama
Manispaa ya Morogoro ambayo ndio imetupa maeneo haya ili kujikwamua kiuchumi,
inakuwaje chama ambacho manispaa hii ni sehemu ya idara zake kinaipuuza manispaa
na kutumia ubabe? Alihoji Lauo na kuendelea: Sisi tuliingia makubaliano na manispaa
kwa nini wao waje baadaye na kuanza kutusumbua mbona hawakuja wakati tumeanza
ujenzi? Huu ni uonevu maana wanatumia nguvu ya chama chao kunyanyasa wananchi,
hatukubali na lazima kieleweke.
Anasema
wafanyabiashara walitumia gharama nyingi kujenga mabanda hayo, hivyo kitendo
cha kunyang’anywa na kuachwa bila shughuli ya kufanya haiwafanyi kuendelea kukiamini CCM, na kusema kwa umoja wao na watu wengine
watakaowashawishi watavipigia kura vyama vya upinzani.
“Hatuwezi
kukichagua chama ambacho kinaleta mateso kwa wananchi wake…kura zetu
hawataziona na msimamo wetu uko pale pale kwamba lazima warudishe mabanda yetu
na gharama tulizotumia kwenye ujenzi.”
Anasema
baada ya banda lake kubomolewa alipoteza mashine za kukoboa mahindi, mpunga na
gunia 100 za mahindi na mali nyingine zilizokuwapo ndani ambazo mpaka sasa
hazijapatikana na kudai kwamba CCM waliziuza.
NINI KILIO CHAO
KWA SERIKALI?
Kilio
chao ni kuona Serikali ikiingilia mgogoro huo kwani wafanyabiashara hao ni
walipakodi wazuri ingawa serikali inatambua changamoto hiyo bila kuchukua
hatua.
Mluge
anasema wana mpango wa kuwasiliana na wanasheria ili kuona haki ya wafanyabiashara
wote inatimizwa.
MKURUGENZI WA
MANISPAA:
Manispaa
ya Morogoro ambayo wafanyabiashara hao wanadai maeneo waliyopokonywa waliyapata
kutoka uongozi wake, Mkurugenzi wa Manispaa
hiyo, Theresia Mahongo anasema hana muda mrefu tangu ahamishiwe kituo
hicho kipya cha kazi lakini atafuatilia na kutoa majibu.
“Ni
kweli sisi ndiyo wenye mamlaka kwenye manispaa hii lakini mimi sina muda mrefu
tangu nihamishiwe hapa, hivyo sina taarifa kuhusu jambo hili, ninachofahamu ni
kwamba sabasaba ni eneo lililotengwa kwa ajili ya wafanyabiashara lakini huo
mgogoro siufahamu…labda nitafuatilia alafu nitakupa majibu,” anasema Mahongo.
Hata
hivyo amewataka wafanyabiashara hao kufika ofisini kwake kwa lengo la
kuwasilisha malalamiko yao na kuahidi kuchukua hatua haraka kwani ni jukumu la
manispaa husika.
MAJIBU YA CCM:
Mwandishi
alimtafuta Katibu wa CCM wilaya ya Morogoro mjini, Ally Issa Ally ambaye
malalamiko mengi yameelekezwa kwake, ambapo akizungumza kwa njia ya simu
alipoulizwa kuhusu suala hilo alijibu kwa mkato kuwa hafahamu kuwa CCM ina
mgogoro na wafanyabiashara.
Majibu
yake ya mkato alipoulizwa na mwandishi yalikuwa hivi:
Mwandishi: Bila shaka wewe
ni ndugu, Ally Issa Ally
Katibu: Ndiye mimi
unasemaje?
Mwandishi: Unatambua
mgogoro baina yenu CCM na wafanyabiashara wadogowadogo pale eneo la Sabasaba?
Katibu: Sifahamu
lolote, kama unahitaji maelezo zaidi njoo ofisini
Mwandishi: Umesema
hufahamu lolote, huko ofisini kuna maelezo gani zaidi?
Katibu: Kisha akakata
simu.
Katibu
mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana hakupatikana kuzungumzia kadhia hiyo baada ya
simu yake ya mkononi kutafutwa mara kwa mara bila kupokelewa au hapatikani
wakati mwingine.
Wakati
wafanyabiashara hao na wengine nchini wakiwa kwenye mazingira magumu kama hayo,
serikali inakiri kuwa sekta ya viwanda vidogo na biashara
ndogondogo zina mchango mkubwa katika ajira kwa takriban ajira 5,000,000 sawa
na asilimia 23.4.
Kwa sasa sekta hiyo imechangia asilimia
27.9 katika pato la taifa ukilinganisha na mwaka 2012/13 ambapo sekta ya
biashara ndondogo na viwanda vidogo imechangia asilimia 12.3.
Serikali kupitia wizara ya viwanda, biashara na
masoko inasema ongezeko la ukuaji na uchangiaji huo umetokana na kuongezeka kwa
fursa mbalimbali za masoko kwa bidhaa na uboreshaji wa mazingira ya kibiashara
katika masoko ya ndani na nje ya nchi hasa kwenye nchi zinazounda Jumuiya ya
Afrika Mashariki, EAC, Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC, Jumuiya ya Ulaya, EU, Asia, Marekani na
mashariki ya mbali. CHANZO: TAIFA LETU
COMMENTS