IGP Ernest Mangu MAPEMA wiki hii, Jeshi la Polisi kupitia Mkuu wa Jeshi hilo (IGP), Ernest Mangu lilisisitiza onyo dhidi ya vya...
IGP Ernest Mangu |
MAPEMA wiki hii, Jeshi la Polisi
kupitia Mkuu wa Jeshi hilo (IGP), Ernest Mangu lilisisitiza onyo dhidi ya vyama
vya siasa, wagombea na wafuasi wa vyama hivyo kujiepusha na vitendo
vitakavyokiuka taratibu za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka
huu.
Katika Mkutano wake na viongozi mbalimbali wa
dini na kisiasa, IGP alisema vyombo vya usalama vimejipanga vyema kuhakikisha
kuwa uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na utulivu licha ya vuguvugu la
ushindani mkali wa kisiasa uliopo.
Alivitaja vyama vya siasa vya Chama
cha Mapinduzi (CCM) na vyama vya upinzani kama vya muungano wa vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NCCR-Mageuzi, Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NLD na Chama cha Wananchi (CUF) kuwa na
ushindani mkubwa wa kisiasa lakini pamoja na uwepo wake, jeshi la polisi
halitarajii kuvunjika kwa amani na utulivu kwa namna yoyote ile.
Ni wazi kwamba kauli ya
kiongozi huyo mkuu wa jeshi ni tahadhari
anayoitoa kwa mamlaka za vyama kuwa makini, utiifu, na ni wazi kwamba kauli
yake hiyo pia ni ombi kwa viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada
kuwahamasisha waumini wao ili kujiepusha na vurugu wakati wa uchaguzi mkuu.
Hii maana yake ni kwamba watakaovunja
sheria, watashurutishwa kutii sheria jambo ambalo kwa uzoefu tunaoupota katika
nchi za jirani ni wazi kwamba ushurutishaji wa sheria umeleta madhara makubwa
ikiwamo vurugu, vita, vifo na wananchi wengine kulazimika kuyakimbia makazi
yao.
Tumeshuhudia kwa kuona,
kusikiliza na kusoma kwenye vyombo mbalimbali vya habari 0kuwa waathirika
wakubwa wa matukio ya fujo na vita ni wanawake, watoto, walemavu na kundi la watu wengine wasiojiweza kama vile wazee.
Tunapohimiza kufanyiwa kazi kwa
onyo la jeshi la polisi, ni pale IGP Mangu anapotoa karipio hilo tunasikia
kwamba wapo viongozi wa vyama
wanaohamasisha mpango wa kuanzisha vikundi
vya ulinzi vya vyama vya siasa kwa madai ya kulinda kura wakati wa uchaguzi wakati
kimsingi jukumu hilo lipo chini ya jeshi la polisi lenyewe.
Maana ya IGP kukemea vyama vya
siasa vyenye malengo hiyo ni kusisitiza wajibu wake kwa jamii kwamba ni kulinda
usalama wa mali na raia wakati na baada ya uchaguzi, hivyo hakuna sababu yoyote ya vyama hivyo kuwa
na vikundi kama vile Green Guard cha CCM, Blue Guard cha Chama cha Wananchi (CUF) na Red Brigade cha Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na hivyo vyama vinapaswa kusitisha harakati
zao kwani ni kinyume cha sheria.
Sisi tunaungana na Jeshi la
Polisi kukema vitendo vya vyote vinavyokiuka taratibu za uchaguzi kutokana na
ukweli kwamba vyama hivyo hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na vyombo vya
usalama vilikubaliana kwa kutiliana saini mambo ya kuzingatiwa wakati wa
kampeni hadi uchaguzi mkuu ikiwamo chama, mgombea au wafuasi wake kutokiuka
sheria na taratibu za uchaguzi na kusababisha kutoweka kwa amani na utulivu
nchini.
Mojawapo ya mambo yaliyoanishwa
na kukubaliwa ni pamoja na kutotumika kwa lugha za uchochezi kwama vile
zinazoshinikiza ushindi, kuchana mabango ya mgombea wa chama kingine na matusi.
Lakini hata baada ya makubaliano
hayo tumeshuhudia matumizi ya lugha za kuudhi, kuchanwa kwa mabango ya
wagombea, vitisho na wagombea kujielekeza katika kusemana wawapo kwenye majukwa
ya kampeni kutoa hoja zitakazowavuta wananchi ili kuwa rahisi katika
utekelezaji wa majukumu yao. Hii yote ni
kufanyika kwa kampeni zisizokuwa za ustaarabu ambazo kwa namna nyingine
huweza kusababisha kukosekana kwa amani na utulivu siyo tu wakati huu wa
kampeni isipokuwa inaweza kutumika kama nongwa wakati wa uchaguzi na kuchafua
hali utulivu.
Sisi tunaamini kwamba kila mmoja
ana wajibu wa kulinda amani na utulivu wa nchi yetu katika kipindi chote cha
kampeni na siku ya uchaguzi mkuu hadi kutangazwa kwa washindi wa nafasi
mbalimbali za uongozi walizoomba wagombea husika.
Hiyo ni pamoja na kutojihusisha
na vikundi vyovyote ambavyo jeshi la polisi limeonya uwepo wake, vinginevyo
jeshi la polisi litalazimika kutumia nguvu kutoa shuruti jambo ambalo ni hatari
kwa usalama na mali zetu.
Pia tunakema tabia ya Watanzania
wanaopenda hulka ya kushurutishwa kutii sheria bila kuzingatia msingi wa utii
wa sheria bila shuruti.
CHANZO: TAIFA LETU
======
COMMENTS