Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Abdulrahman Kinana Na Komba Kakoa RAFU zinazoendelea kulalamikiwa na makada mbalimbali wa Ch...
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Abdulrahman Kinana |
Na Komba Kakoa
RAFU zinazoendelea kulalamikiwa na makada mbalimbali
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni matokeo ya Mamlaka husika kuacha utaratibu wa
enzi ya chama hicho wakati wa Muasisi wake na wa Taifa, Mwalimu Julias Nyerere
na kuanzisha mfumo ambao ni wazi kwamba utazika chama hicho.
Rafu hizo zinalenga kunufaisha baadhi ya makada
ambao kwa maslahi binafsi watangaza nia wasiokuwa wadilifu hutumia mbinu
mbalimbali za kuwahujumu wapiga kura ili waweze kuwachaguwa.
CCM iliyokuwa katika uongozi wa Hayati Baba wa Taifa
hili ni tofauti na CCM ya leo kwasababu mbalimbali ambao kimsingi ni wazi
kwamba kipo kwa ajili ya kunufaisha baadhi ya makada.
Kwamba
katika kipindi cha nyuma viongozi wa chama hicho walikuwa waadilifu na wenye
kuwajibika ipasavyo katika nafasi zao tofauti na ilivyo kwa baadhi ya makada
kujipenda wenyewe na hata kufikia hatua za kukashifiana wenyewe pamoja na chama
hicho jambo ambalo halileti picha nzuri.
Mintarafu yangu kwa leo ni kuhusiana na gharama
mbalimbali za uchaguzi ambazo watia nia hutakiwa kuchangia katika hatua
mbalimbali ikiwemo kuchukua fomu pamoja na gharama za kuwezesha kampeni na
uwakilishi.
Hapo awali chama kilibeba jukumu la kusimamia
mchakato mzima wa uchaguzi kuanzia ngazi ya uchukuaji wa fomu, kampeni, ulipaji
wa mawakala pamoja na kuwezesha usimamizi wa mambo yote katika utekelezaji wa
shughuli hiyo.
Lakini leo mambo ni tofauti kwa uchukuaji wa fomu
kwa nafasi ya urais wanatozwa kiasi cha shilingi milioni moja, Ubunge sh. Laki
moja na ngazi ya Udiwani ikitegemeana na makubaliano ya makada wa kata husika.
Mbali na gharama hizo pia kuna michango ya kuwezesha
kampeni ambapo mtia nia huyo huyo anapaswa kulipa mawakala wake wanaosimamia mchakato wa
kuhesabu kura hali ambayo inamnyonya na kumnyima haki Mtanzania mwenye sifa na
nia ya kuwania nafasi ya uongozi kwasababu ya gharama hizo ambazo awali
hazikuwepo.
Kwa upande mwingine uwepo wa michango hiyo ni furaha
kwa makada wenye uwezo hasa zaidi waliokuwa kwenye madaraka kwasababu wana
marupurupu mengi yanayowafanya wamudu gharama hizo na kuwapa fursa ya kuwapiku
wasiokuwa nacho.
Katika mchakato wa kura za maoni tuemeshuhudia
mpasuko ndani (CCM) kutokana na uwepo wa makundi yaliyosababishwa na makada
wenye uwezo kifedha na nguvu katika chama hicho jambo ambalo kimsingi halina
tija kwa maendeleo na uwajibikaji katika kutekeleza ilani.
Yote hayo ni matokeo ya CCM kupitisha utaratibu wa
mtangazania kugharimikia mchakato, swali linalosumbua vichwa vya Watanzania
hasa wana CCM ni kwamba kwanini chama hicho kimeondoa ule utaratibu wa kubeba
dhamana ya watia nia wote?
Kwamba katika wakati ule CCM ilibeba dhamana ya
kufadhili watangazania wote kwa gharama zote za uchaguzi jambo ambalo
liliimarisha chama na sote tulishuhudia umoja na uwajibikaji wa makada walipata
fursa ya kuchaguliwa na kushika majimbo pamoja na kata mbalimbali hapa nchini.
Kutokana na utaratibu wa kila mtangazania kuchangia
gharama za uchaguzi unaendelea kuleta madhara kwa wasionacho kufunikwa na
kufanyiwa rafu za hapa na pale katika mchakato mzima wa kura za maoni.
Kwa makada waliotangaza nia walitembezwa pamoja kwa
usafiri wa aina moja ili waweze kuonekana kwa wananchi na kupata fursa ya
kujinadi na kuomba kura tofauti na ilivyo katika kipindi hiki ambacho kila mtia
nia alisafiri kivyake na kwa utaratibu wake.
Katika kura za maoni tumeshuhudia makada wenye nacho
wakikodisha mabasi na kuyabandika picha zao ‘stika’ na kuzunguka nayo sehemu
mbalimbali kwa dhumuni la kujinadi.
Mbali na waliofanya hivyo wengine waliamua kukodisha
vijana waendesha pikipiki `Bodaboda’ na kuwajazia mafuta na kuwapa kazi ya
kuzunguka kwenye matawi ya CCM kwa lengo la kushawishi wapiga kura wawachague
makada hao.
Mbali na hayo katika kufanya kampeni pia ni wazi
kwamba katika kipindi cha nyuma hakukuwa na utaratibu wa kutangaza nia kwa
makada jambo ambalo limeibuka na kusababisha baadhi ya makada kutumia mwanya
huo kuanza kufanya kampeni kabla ya wakati.
Kwa hali hiyo ni vyema CCM ikarudia enzi yake na
kuachana na mfumo ambao ni utazidi kudidimiza demokrasia ya nchi yetu pamoja na
kuathiri zaidi watangaza nia wenye uchungu na changamoto za wananchi na
kuwainua mabepari wenye uchu wa madaraka wanaodiriki kutumia rafu ilimradi tu
wapate madaraka.
==============
COMMENTS