Na Felix Kalisa NIMESHANGAZWA na habari moja iliyoandikwa kwenye gazeti moja la kila siku ikiwataka wabunge wa Chama Cha Mapinduzi...
Na
Felix Kalisa
NIMESHANGAZWA
na habari moja iliyoandikwa kwenye gazeti moja la kila siku ikiwataka wabunge
wa Chama Cha Mapinduzi, CCM kuhakikisha wanaibana serikali inayotokana na chama
chao, ili itekeleze ilani na kuziba mianya ya ubadhirifu wa fedha za umma.
Kwa
mujibu wa gazeti hilo ni kwamba; Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana ndiye aliyetoa
wito huo kwenye semina ya siku mbili ya wabunge wanaotokana na chama hicho,
iliyofanyika hivi karibuni mjini Dodoma.
katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana |
Hatua
hiyo inadaiwa imelenga kuhakikisha wabunge wa vyama vya upinzani wanakosa
kabisa hoja za kuikosoa bungeni na hatimaye kuidhohofisha kiutendaji Serikali
ya Chama Cha Mapinduzi, inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.
Kwa
mujibu wa habari hiyo; Kinana anadai wabunge wa vyama vya upinzani wamekuwa
wakiibana serikali kwa kuikosoa na kufichua mianya yote ya ufisadi inayofanywa
na viongozi mbalimbali wakiwa madarakani.
Katika
kikao hicho kilichoanza chini ya Kinana, kilidaiwa pamoja na mambo mengine kuwa
na ajenda tatu ambazo ni Wajibu wa wabunge wa CCM kwa serikali, Tathmini ya
Uchaguzi Mkuu uliopita na mchakato wa kura za maoni ndani ya chama.
Nasema
nimeshangazwa na habari hiyo kwa sababu kuu moja; Ukiondoa utawala wa awamu ya
kwanza, enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na kabla ya ujio wa
serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. Magufuli; kitendo cha
wabunge wa CCM kuthubutu kukikosoa chama ama kufichua mianya ya wizi, rushwa na
ufisadi unaofanywa na viongozi ni sawa na usaliti!
Hata
vyombo vya habari vinavyomilikiwa na chama navyo vilijikuta vikinasa katika
kasumba hiyo mbaya ya kusifu tu bila kukosoa kana kwamba Tanzania ni mbinguni
na watawala ni miungu na malaika wasiofanya makossa.
Ni
katika mazingira kama hayo ndipo inasemekana wabunge wengi wa CCM wamekuwa
wakilazimika kusifu tu na kupongeza kila jambo linalofanywa na chama chao, hata
kama halina tija kwa umma na serikali huku pia wakisimama kidete kwa nguvu zote
kupinga ukosoaji wowote ule dhidi ya serikali na chama chao hata kama ukosoaji
huo una ukweli kwa asilimia mia moja!
Ndiyo
maana sikushangaa kuwaona baadhi ya viongozi waandamizi, wabunge na makada
‘wazalendo’ wa chama hicho; waliowahi kuthubutu kukosoa ama kuibua kashfa dhidi
ya wenzao ndani ya chama na serikali, wakiitwa wasaliti na waasi au wakiitwa
kujadiliwa na kuhojiwa katika vikao vya juu vya chama; huku pia baadhi yao ama
‘wakiundiwa zengwe’ la kuangushwa kwenye uchaguzi kupitia kura za maoni ndani
ya chama, ama wakati mwingine wakinyang’anywa uanachama na kufukuzwa.
Miongoni
mwa waliowahi kukumbwa na dhahama kama hizo; ni pamoja na aliyewahi kuwa Katibu
Mkuu wa chama hicho, Hayati Horace Kolimba baada ya kutofautiana na mwenendo
mbovu wa chama chake na kuanika bayana kuwa chama hicho kimekosa dira na
mwelekeo; Kolimba alifariki dunia mjini Dodoma Machi 13, 1997 muda mfupi baada
ya mahojiano makali ndani ya vikao vya juu vya chama.
Mwingine
ni mkongwe na muasisi wa mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 na mwanachama
wa CCM mwenye kadi namba 7, mzee Hassan Nassor Moyo aliyetimuliwa kwa
kosa la kukosoa muundo wa muungano wa serikali mbili, ambao (kwa uhuru wake wa
kutoa maoni kwa mujibu wa katiba ya nchi) anaona muundo huo hauna tija na
umepitwa na wakati.
Mwingine
pia aliyewahi kufukuzwa uanachama kwa sababu inayofanana na hiyo ya Mzee Moyo;
ni aliyewahi kuwa Waziri Mwandamizi chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Zanzibar, (SUK) na mwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki Mansour Yusuf Himid;
achilia mbali baadhi ya wabunge machachari wanaodaiwa kutazamwa vibaya ndani ya
chama kwa misimamo na uthubutu wao wa kuhoji, kukosoa na kukemea maovu ya
viongozi ndani ya chama na serikali.
Hao
ni pamoja na aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Ludewa (CCM) Hayati Deo
Filikunjombe, Mbunge wa Simanjiro (CCM) Christopher Ole Sendeka, aliyewahi kuwa
Mbunge wa Jimbo la Kahama (CCM) James Lembeli, aliyewahi kuwa Mbunge wa viti
maalumu (CCM) Bunda mjini kabla ya kuhamia Chadema na kuwa Mbunge wa
kuchaguliwa wa jimbo hilo, Esther Bulaya; nawataja kwa uchache tu.
Nasema
hivyo nikiwa na kumbukumbu ya mijadala ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuhusiana na kashfa mbalimbali zilizowahi kulikumba taifa letu na
kulisababishia hasara kubwa ya mabilioni kwa matrilioni ya fedha ambazo
zingetumika kulivusha taifa mbali sana kiuchumi na kijamii.
Kashfa
hizo ni pamoja na ile ya wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Kashfa ya
mkataba wa kifisadi kati ya Shirika la Ugavi wa Umeme nchini, Tanesco na
Kampuni ya kuzalisha umeme ya Richmond Development (LLC), sakata la wizi wa
fedha za akaunti ya Tegeta Escrow, kashfa ya manunuzi ya Rada, Utoroshwaji
wanyama, ujangili, madawa ya kulevya, akaunti tata za siri huko ughaibuni n.k.
Tulishuhudia
migogoro yote hiyo ikifanyika ndani ya bunge letu kwa picha ya mapambano ya
wabunge wa CCM waliokuwa wakiwawekea kifua watuhumiwa kwa kuwasafisha kadri
walivyoweza, dhidi ya wabunge wachache wa upinzani waliotaka hatua kali
zichukuliwe kwa mujibu wa sheria za nchi.
Hivyo
basi badala ya wananchi kushuhudia wabunge wazalendo wa Tanzania bila kujali
itikadi zao za vyama wakipambana dhidi ya wahalifu na uhalifu, wakajikuta
wakishuhudia mapambano kati ya wabunge wa CCM dhidi ya wale wa upinzani hali
iliyotafsiriwa kama vita ya CCM na Ukawa badala ya vita ya Bunge la Tanzania
dhidi ya uhalifu na wahalifu.
Sasa
sijui kama Bunge hili la 11 (hasa kwa
wabunge wa CCM), chini ya utawala wa awamu ya tano ya Rais Dk. Magufuli,
litaweza kufanyia kazi maagizo hayo ya Katibu Mkuu wa CCM (taifa), Comrade Kinana
ya kukosoa, kuibua maovu, kukemea na kuisimamia serikali kama wafanyavyo
wabunge wa Ukawa.
Ni
kwa njia hiyo pekee vyama vya upinzani vinaweza kudhohofishwa kisiasa bungeni
na mbele za wananchi; kwa sababu kinachowafanya wao na hoja zao kuwa na nguvu
ndani na nje ya bunge, ni kulinda na kutetea maslahi ya umma na taifa zaidi
kuliko kuendekeza uchama.
Naweza
kusema hiyo ndiyo tofauti kubwa kati ya wabunge wa CCM na wale wa vyama vya
upinzani, kuhusiana na suala zima la wajibu wa bunge katika kuishauri na
kuisimamia serikali kikamilifu, ili mapato yatokayo na kodi na utajiri mkubwa
wa rasilimali za nchi, yaweze kuifaa nchi na wananchi wote bila kujali itikadi
zao.
Lakini
hoja ambayo Kinana anatakiwa kujiuliza ni kwanini anayoagiza wabunge wa CCM
katika Bunge hili hayakutekelezwa katika bunge la 10, ili-hali yeye na timu ya
viongozi wenzake walifanya ziara kwenye mikoa mbalimbali na agenda kuu ya
mikutano ya ziara hizo ilitawaliwa na karipio dhidi ya viongozi wa umma na hata
ikafikia kuwaita baadhi ya mawaziri waliotokana na CCM kuwa ni mizigo? Tungoje
tuone wabunge wa CCM wenye ujasiri wa kutekeleza kile anachotaka Kinana.
Ni
muhimu pia kutambua kuwa changamoto hii inayotolewa na Kinana kwa wabunge wake
ni juhudi ya wapinzani kuibua uovu wa viongozi, lazima Kinana atambue kuwa
wapinzani nao watakuja na mipango na mikakati yao mipya.
0655
872873, 0784 872873.
==============
Imetumika TAIFA LETU
COMMENTS