Sehemu ya kuku wa aina mchanganyiko, RHODE ISLAND RED na KUROILER wanaofugwa katika shamba la mradi wa RABIKA POULTRY FARM Kata ya...
Sehemu ya kuku wa aina mchanganyiko, RHODE ISLAND RED na KUROILER wanaofugwa katika shamba la mradi wa RABIKA POULTRY FARM Kata ya Kibamba, Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani (Picha TTAJA).
Na Komba Kakoa na Eligius Nyoni
“NI
kijiji katikati ya pori, lakini wanyama wake ni kuku. Tofauti yake ni kwamba
majengo yake yameezekwa kwa mabati, tena kwa unadhifu mkubwa sana. Tunaposogea
zaidi, tunakaa kwenye nyumba ya msonge, macho yanaanza kupepesa huku na kule,
pamependeza mno, ni kijani kibichi, mmoja wetu anasimama na kutupa macho mbali na kuibuka na maneno, he! Kumbe hii ni ranchi ya kuku, wengine tukaangua kicheko,” ni kauli ya mmoja wa wajumbe wa timu ya waandishi wa habari wa chama cha waandishi wa habari za vijijini (TTAJA) waliotembelea shamba la ufugaji kuku, kikiji cha Rabika, Kata ya Kibamba wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
pamependeza mno, ni kijani kibichi, mmoja wetu anasimama na kutupa macho mbali na kuibuka na maneno, he! Kumbe hii ni ranchi ya kuku, wengine tukaangua kicheko,” ni kauli ya mmoja wa wajumbe wa timu ya waandishi wa habari wa chama cha waandishi wa habari za vijijini (TTAJA) waliotembelea shamba la ufugaji kuku, kikiji cha Rabika, Kata ya Kibamba wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
“Msisitizo
mkubwa unaowekwa na serikali ni watu kuwa na mawazo ya kujiajiri, tupo ambao
tumeanza kuthubutu kwakutambua kwamba serikali haina uwezo wa kuajiri kila mtu,
jambo la kustaajabu ni pale wale tulioanza kuthubutu tunakosa ushirikiano kutoka
kwenye mamlaka serikalini,” hiyo pia ni kauli ya Hamid Abdullkarim, meneja wa shamba
hilo akifungua pazia la ziara hiyo.
Abdullkarimu,
anasema pamoja na changamoto hiyo mpango wao ni kuongeza uzalishaji na masoko,
kupanua mradi kwa kuanzisha shamba jipya na vitendea kazi muhimu ili kufikia
malengo ambayo kiasi fulani wameanza kuyachungulia.
Meneja
huyo aliiambia timu ya waandishi wa habari wa chama cha waandishi wa habari za
vijiji cha Tanzania Transparency Journalists Association (TTAJA) waliotembelea
mradi huo Agosti 21 mwaka huu kuwa walianza mradi huo baada ya kufanya utafiti
wa aina za kuku wanaomudu mazingira yote na pia kulingana na soko.
“Tulifanya
utafiti wa awali mwaka 2009 kabla ya kuanza kwa mradi mwaka 2010.Utafiti
ulijumuisha aina za kuku kwenye mataifa mengine ya nje ambao wakichanganywa
wanaweza kuuzika katika soko la ndani na nje,”anasema.
Meneja wa shamba la Rabika Poultry Ahmed Abdullkarim |
Anasema
utafiti huo ulionyesha kuwa aina bora ya ufugaji wa kuku ni ile ya Nusu Huria ambayo uzalishaji
licha kutumia gharama nafuu, inastahimili magonjwa, kuku kuishi kwenye
mazingira ya aina zote ulinganisha na aina ya kisasa zaidi (Commercial broiler)
ambayo pamoja na kutumia gharama kubwa, nyama ya kuku wa aina hiyo imekuwa na
changamoto nyingi, ikiwamo walaji kukimbia nyama yake kwa kuhofia kemikali
zinazotumika katika uzalishaji.
Ufugaji
huria katika shamba hilo linalotambulika kama Rabika Poutry Farm hujumuisha
aina ya kuku wanaotambulika kitaalamu kama New Hamshire wenye rangi nyekundu kutoka nchini Burundi wenye asili ya
Uingereza.
Anasema
aina hiyo hutumika kwa ajili ya nyama na mayai wenye uwezo wa kukua kwa uzito
wa kilogramu 2 hadi 4, hutaga mayai
kuanzia 140 hadi 200 kwa mwaka.
Aina
nyingine ni Rhode Island Red pia wa rangi nyekundu ambao uzalishaji wake
ulianzia nchini Uholanzi mwaka 1961. Aina hiyo hukua na kufikia wastani wa kilo
2 hadi 2.5 na hutaga mayai 200 hadi 250 kwa mwaka na yana uzito wa gramu 45
hadi 100 kwa mwaka.
Anazitaja
aina nyingine kuwa ni Kuroiler zenye rangi mchanganyiko kutoka Uganda wenye
asili ya India ambao hufugwa kwa ajili ya nyama na mayai, hutaga mayai kati ya
150 hadi 250 yenye ukubwa wa gramu 45 hadi 80. Aina hiyo ya kuku hunenepa na
kufikia kilo 2 hadi 4.
Pia
wanafuga kuku aina ya Black Austrolop (wenye rangi nyeusi) kutoka nchini Malawi ambao hufugwa kwa ajili ya mayai,
hutaga mayai kati ya 200 hadi 250 kwa mwaka yakiwa na ukubwa wa gramu 45 hadi
75.
MAFANIKIO:
Meneja
huyo wa Shamba la Rabika anasema wakati wanaanza mradi huo mwaka 2010 walianza
kwa mtaji mdogo wa kufuga wazazi (Parent stock)
kuanzia ngazi ya vifaranga 300 ambapo waliweza kuwakuza na kufikia
kiwango cha kutaga.
Waliweza
kuongeza uzalishaji huo mara dufu kwa kiwango cha wazazi 600 na kutumia
mafanikio hayo kununua mashine za utotoleshaji wa vifaranga kwa mayai
waliyokuwa wanazalisha kupitia idadi hiyo ya wazazi.
“Baada
ya kununua mashine za utotoleshaji tulifanikiwa kuongeza zaidi mazao na kufikia
kuku 1,236 kwa kipindi kifupi sana…ongezeko hilo lilitutia faraja, ambapo
tuliongeza kuku 800 zaidi na kufikia idadi ya
kuku 2,000 wa aina tofauti tofauti,”anasema Abdullkarim.
Anasema
ufugaji wa kuku kwa mfumo wa Nusu Huria, huzingatia kanuni za kitaalamu na
maelekezo mengine una tija katika soko la ndani na nyama, na kushauri jamii
kuhama kwenye mfumo huria ambao kuku wengi hudumaa kutokana na kukosa lishe
sahihi na magonjwa.
Kwa
hali hiyo, jamii ya wakulima wamekuwa wakifuga kwa mfumo ambao hauna tija jambo
ambalo husababisha jamii husika kutofikia malengo ya ufugaji, anasema.
Anasema
sehemu kubwa ya wakulima na jamii nyingine barani Afrika zimeachana na ufugaji
huria wa kuku na kujiunga na mfumo wa nusu huria akitolea mfano wa nchi kadhaa
kama vile Malawi, Uganda, Burundi na Rwanda kwa kusema kuwa zimepiga hatua
kubwa kimaendeleo kupitia nyama ya kuku baada ya kujiunga na mfumo wa nusu
huria.
Ufugaji
kuku wa Nusu Huria umekuwa na mafanikio makubwa kwa wao wa kuku wa kuku kwa
mtindo wa nusu huria, ni mfumo ambao mfugaji hutumia mbinu za kitaalamu katika
ulishaji kwa mfumo usiotofautiana sana na ule wa huria. Kuku wanaofugwa katika
mfumo huo huwekwa kwenye kizuizi kama ilivyo mfumo wa kisasa ingawa
hutofautiana kidogo na mfumo kisasa (broiler) ambao wakati wote kuku
huhifadhiwa bandani. Mfumo wa Nusu Huria huwawezesha kuku kuishi kwa kula na
kutoka nje ya mabanda kwenye eneo la wazi lililotengwa kwa nyavu jambo ambalo
kwa mazingira ya kuku wa kisasa (broiler) siyo rahisi kuishi.
Pia
mfumo wa Nusu Huria kuku huweza kuwa mabandani wakati wa kulala (usiku) baada
ya kuwa nje ya mabanda kwenye eneo maalumu lililotengwa kipindi chote cha mchana.
Pia uzalishaji wa Nusu Huria hutofautiana kidogo na mfumo wa kuku wa Broiler.
“Tumefanikiwa
kutoa ajira kwa vijana sita ambao tunasaidiana nao katika kuhudumia mifugo yetu
kila siku kwa chakula na dawa na kuhakikisha mradi wetu unaimarika,”anasema.
MIPANGO YA
BAADAYE:
Anasema
pamoja na changamoto zilizopo, mpango wao ni kuongeza uzalishaji zaidi, kuwa na
mashine yao wenyewe ya kuzalisha chakula
cha kuku badala ya kununua chakula kwenye maduka ya vyakula vya kuku ambacho
hatuna uhakika nacho kutokana na wazalishaji wasiokuwa waaminifu.
“Tayari
tumejenga kituo cha uzalishaji…hivi sasa tupo kwenye mchakato wa kuweka mashine
ya kusindika chakula ili tuachane na kununua chakula ambacho hatuna uhakika na
utengenezwaji wake, ambao mara nyingi umekuwa ukitutia hasara tukiamini kina
virutubisho, kumbe kimechakachuliwa… ni kuhatarisha afya ya kuku,”anasema.
Anasema
wamewasiliana na uongozi wa wilaya kwa ajili ya kufikisha ombi kwa wakala wa
nishati ya umeme vijijini (REA) ili kufungiwa umeme ambao umeishia kijiji cha
Kibamba, kilometa tatu kutoka kijiji cha Rabika ulipo mradi huo.
Anasema
uongozi mzima wa Wilaya hiyo uliwahi kuongozana na Mwenge wa Uhuru na kufika kwenye mradi huo na kufanikiwa
kufungua jengo la utawala la shamba hilo, ambapo viongozi mbalimbali akiwamo
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga waliahidi kushirikiana nao kwa lengo ka kuondoa
changamoto zinazowakabili, ikiwamo tatizo hilo la umeme.
Anasema
Mkuu wa wilaya hiyo amekuwa akiwatembelea mara kwa mara, kuwapongeza na
kuwaahidi kushirikiana nao, kuhamasisha jamii kwenda kufika kwenye shamba hilo
na kujifunza mbinu za ujasiriamali ambapo yeye mwenye (Mkuu wa Wilaya) amechukua
vifaranga ili kuanza ujasiriamali huo kama mfumo kwa wanajamii wengine.
Mipango
mingine ni pamoja na kuongeza mtaji wa
Shilingi milioni 200 kutoka mtaji wa sasa wa milioni 100 ili kufikia malengo ya hitaji la mtaji uwekezaji wa Sh.miilioni 300 kufikia
malengo ya uzalishaji zaidi katika shamba jipya la ekari 50 huko kijiji cha Kisegese, na shamba
la sasa litatumika kama kituo cha usambazaji na majaribio.
Pia
aliwaambia waandishi hao wa TTAJA kuwa mipango yao mingine ambayo utekelezaji
wake unaanza mwaka 2016 ni pamoja na kuwa na mashine za kunyonyoa, kuongeza
uzalishaji wa nyama ya kuku tani 5 hadi 10 kwa siku, kuwa na gari lenye deep
freezer (storage van), mashine za kufungashia, duka la nyama, kuongeza kuku
(wazazi) kufikia 5,000 kutoka wastani wa sasa wa wazazi 2000 na kuongeza
uzalishaji wa mayai kutoka trai 15 kwa siku sasa.
CHANGAMOTO:
Changamoto
mojawapo ni hitaji kubwa la nyama ya kuku wa ufugaji wa nusu huria ukilinganisha na kiwango cha nyama
inayozalishwa. Anasema kwa sasa wateja wao wakubwa ni wafugaji wadogo ambao
wamekuwa wakifika kituoni hapo na kufundishwa mbinu mbalimbali za ufugaji,
ingawa mpango wao ni kuwafikia wafugaji wakubwa, hoteli kubwa za kisasa kwa
ajili ya nyama.
Changamoto
ushirikiano mdogo kati yao na baadhi ya viongozi kwenye idara za serikali kwa
maelezo kuwa kumekuwa na ukiritimba pindi wanapofika kwa ajili ya kutafuta
ushauri wa kitaalamu.
“Tumekwenda
pale wizarani, lakini kila wakati ni kusumbuliwa…katika halmashauri pia wapo
maofisa ugani lakini hata mmoja sijawahi kumuona amefika hapa na kututembelea
ili kuona juhudi zetu katika kuisaidia serikali kutoa ajira…mambo haya
hayapendezi hata kidogo,”anasema Abdullkarim.
Kwa
upande wake meneja wa Utawala na Masoko wa mradi huo, Zahor Zahor anasema tatizo
la hawa watafiti wa kuku hapa nchini ni
tatizo.
“Hili
ni tatizo kubwa, ni lazima serikali yetu izinduke sasa na ione umuhimu wa sekta
ya kuku katika kuchangia ajira kwa kuwabaini watafiti wa kuku na kuwatumia…kwa
kufanya hivyo ni lazima sekta hii itakuwa kwa haraka na bila shaka kutakuwa na
ushindani sawa wa soko la nyama kama ilivyo kwenye nchi nyingine,”anasema
Zahor.
Naye
mfanyakazi mkuu wa shamba hilo, Magambo Fanuel anasema kumekuwa na mafanikio
makubwa kwa vijana wanaozunguka mradi huo, licha ya baadhi yao kutopenda kujishughulisha
hasa kwa shughuli za maeneo ya vijijini.
Fanuel
anasema vijana wengi wametembelewa na uongozi wa mradi na kuelezwa manufaa
ikiwa watafika na kufundishwa mbinu za ufugaji kwa maisha yao ya baadaye, hata
hivyo ni vijana wanne waliofika na kufundishwa ingawa kijiji hicho na kile cha
jirani cha Kibamba kina vijana wengi.
“Hii
inasikitisha sana, vijana wanatakiwa kutambua kwamba siyo wakati tena wa
kuchagua kazi…naaamini kwamba kama wangejitokeza kwa wingi wakafika hapa
wangepatiwa mafunzo…kisha wakapatiwa vifaranga vya kuanzia ni lazima
watabadilika kiuchumi na kujipatia ajira,”anasema.
Msimamizi
huyo wa shamba anasema: “Hiki sio kipindi cha vijana kutegemea ajira kutoka
serikalini ila wanapaswa kuthubutu na kuhakikisha wanajituma kwa bidii ili waweze
kujikwamua katika wimbi la umasikini,” anaongeza.
Anasema
amepata manufaa makubwa tangu ajiunge na mradi huo mwaka jana ambapo ameweza
kusomesha watoto wake, mmoja shule ya sekondari Makongoro na mmoja shule ya
Msingi Busore, wilayani Bunda mkoa wa Mara.
COMMENTS